Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Job Ndugai akiagana na Rais
CPA-Afrika Dkt. Acho Ihim mara baada ya kufunga mkutano wa Chama hicho Jijini
Dar es Salaam.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Job
Ndugai ameahidi kudumisha ushirikiano na Chama cha Wabunge wa Jumuiya ya Madola-Kanda
ya Afrika.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam na Wajumbe wa Kamati Tendaji
ya chama hicho Mhe Ndugai amesema amekuwa Kiongozi na ameshiriki kwa muda mrefu
katika shughuli za chama hicho na hivyo anaelewa mchango wa chama hicho katika
kusaidia kusukuma mbele ajenda za Bara la Afrika katika Jumuiya ya Madola.
“Nipo pamoja nanyi na nimefanya kazi pamoja na Vingozi
wengine katika Chama hiki katika kuzipeleka mbele ajenda za Bara la Afrika
katika Jumuiya ya Madola,” alisema Mhe Ndugai.
Spika Ndugai aliongeza kuwa kwa kadri ambavyo Wabunge wapya wamekuwa
wakichaguliwa ni vyema Wabunge wao wakaendelea kuelimishwa juu ya umuhimu wa
Vyama vya Kibunge ikiwemo Chama cha Wabunge wanachama wa Jumuiya ya Madola ili
waweze kusaidia katika kusukuma mbele ajenda za bara la Afrika katika Vyama
hivyo.
“Ninawahakikishia pia ushiriki wa Wabunge kutoka Bunge la
Tanzania katika shughuli mbalimbali za chama hichi ikwemo Mkutano ujao wa 62 wa
Chama cha Wabunge wanachama wa Jumuiya ya Madola,” alisema Spika Ndugai.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Tendaji wa CPA-Afrika
Mhe Lindiwe Maseko alimshukuru Mhe Ndugai kwa ushirikiano ambao Bunge la
Tanzania limeendelea kuonesha katika shughuli mbalimbali za CPA.
“Tunashukuru kwamba Tanzania imeendelea kuwa mwanachama hai
wa CPA-Kanda ya Afrika na nimatumaini yetu kuwa mtaendelea kudumisha moyo huo,”
alisema Mhe Maseko.
|