SERIKALI imewasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na
Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha, 2017/18 ambapo imepanga
kutumia Sh. Trilioni 31.6.
Taarifa hiyo imewasilishwa Bungeni
leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika
Mkutano wa Wabunge wote kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Bunge.
Dk. Mpango alisema kati ya kiasi hicho kilichopangwa kutumiwa, fedha
zinazotokana na Mapato ya Ndani ni Sh. Trilioni 19. 9 sawa na asilimia
63 huku washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. Trilioni 3.9
sawa na asilimia 12. 6 na fedha nyingine ni mikopo kutoka soko la ndani.
Aidha, alisema Serikali inatarajia kutumia Sh. Trioni 19.7 kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na Sh. Trilioni 11. 9 kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
Akibainisha baadhi ya maeneo ya kipaumbele katika
bajeti ya mwaka 2017/18, Dkt. Mpango alisema ni pamoja na ujenzi wa reli
ya kati, kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania, ujenzi wa mgodi wa chuma
na Kiwanda cha Chuma Liganga Njombe na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma.
“Vipaumbele vingine ni uanzishwaji wa Kanda Maalum ya Kiuchumi Tanga,
Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara, kuendeleza Mradi wa Liquified
Natural Gas, kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Makao Makuu Dodoma na
kuendeleza Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi,” alisema.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai aliiagiza Kamati ya
Bajeti kuyafanyia kazi mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Serikali na
kuzishauri Kamati za Bunge za Kisekta na Serikali.
“Vilevile mara
baada ya kupokea mapendekezo haya, Kamati zote ziandae ratiba ya
kuchambua Bajeti za Wizara wanazozisimamia na kazi hii imalizike kabla
ya kuanza kwa Mkutano wa Saba wa Bunge kwa kuwa haiahirishiki,” alisema.
Aidha, aliwataka Mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wa Serikali
kuhakikisha wanashilikiana na Kamati katika uchambuzi wa bajeti za
wizara zao.
No comments:
Post a Comment