Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai akionyesha ripoti ya uchambuzi wa bajeti za lishe kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika aliyoizindua katika ukumbi wa Msekwa, Bungeni, Jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Wabunge Vinara wa lishe, usalama wa chakula na haki za Watoto Bungeni Mhe. Dustan Kitandura, Mtaalam mwandamizi wa lishe kutoka Mradi wa ASPIRES, Tumaini Charles na kulia kwake ni Mkurungenzi Mtendaji PANITA, Tumaini Mikindo.
HALMASHAURI ZASHAURIWA KUONGEZA FEDHA KATIKA BAJETI ZA LISHE
Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ameshauri Halmashauri nchi kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya masuala ya lishe kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano katika Bajeti zijazo kwa sababu fedha zinazotengwa sasa bado hazikidhi mahitaji yote.
Mhe. Ndugai aliyasema hayo jana wakati akizindua ripoti ya uchambuzi wa bajeti za lishe kwa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika nchini katika mkutano wa wabunge vinara wa lishe, usalama wa chakula na haki za watoto Bungeni ulioandaliwa na taasisi zinayoshughulika na lishe za Panita na Mradi wa lishe wa Aspires uliopo chini ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID).
Mheshimiwa Spika Ndugai alisema ingawa bado kiwango hicho hakikidhi mahitaji yote ya watoto lakini ni hatua nzuni na kushauri kuendelea kuongeza kiwango katika bajeti zijazo.
“Ni wito wangu kwa TAMISEMI (Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa) kuhakikisha kuwa fedha hizo zinazotengwa katika bajeti za halmashauri zinatolewa kikamilifu na kwa wakati,”alisema.
Kwa upande wake Mtaalam Mwandamizi wa Lishe katika Mradi wa Asprires, Tumaini Charles alisema kuna kasi ya ongezeko la watu wenye uzito na kiriba tumbo na kuongeza kuwa tatizo hilo lipo kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye elimu ya sekondari na kuendelea na familia zenye maisha mazuri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANITA, Tumaini Mkindo alishauri Serikali kuangalia jinsi ya kuweka pamoja mipango ya afua za udumavu na uzito mkubwa kwa sababu mtoto aliyekabiliwa udumavu kuwa katika uwezekano wa kupata magonjwa mengine kama ugonjwa wa moyo.
Mwenyekiti wa kikundi hicho Mhe. Danstun Kitandula alisema ni vizuri fedha zinazotengwa kwa ajili ya afua za lishe kuwekewa uzio ili zisitumike katika shughuli nyingine.
“Fedha zinazotengwa kwa ajili ya lishe huwa hazikaguliwi na CAG (Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) tunashauri aweke jicho lake kwenye eneo hilo kwa sababu athari yake ni kubwa,” alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment