WELCOME TO TANZANIA NATIONAL ASSEMBLY OFFICIAL BLOG: CONTACT US: P.O.BOX 941 DODOMA, TANZANIA, WEBSITE: parliament.go.tz , FIND US ON FACEBOOK >>> www.facebook.com/bungetz1, FOLLOW US ON TWITTER >>> @bunge_tz.>>>KARIBUNI

Monday, May 30, 2016

AZIMIO LA BUNGE KUHUSU WABUNGE WALIOFANYA VURUGU BUNGENI JANUARI 27, 2016.

Mhe George Mkuchika Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge akisoma Azimio la Bunge kuhusu Wabunge waliofanya vurugu Januari 27, 2016 Bungeni Mjini Dodoma.

AZIMIO LA BUNGE KUHUSU ADHABU KWA WABUNGE WALIOFANYA VURUGU BUNGENI NA KUDHARAU MAMLAKA YA SPIKA KATIKA KIKAO CHA PILI CHA MKUTANOWA PILI WA BUNGETAREHE 27 JANUARI, 2016

[Limetolewa chini ya Kifungu cha 30A (1) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 74 (4) na (6)]

Kwa kuwa, Bunge letu linaongozwa kwa Mujibu wa Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo tulizitunga sisi wenyewe kwa ajili ya kutuongoza  katika kutekeleza shughuli za Bunge.

Na Kwa kuwa, Sheria na Kanuni hizo zimeweka masharti kuhusu utaratibu unatakiwa kufuatwa katika majadiliano Bungeni na kwamba katika majadiliano hayo, Wabunge wanapaswa kuheshimu na kutii mamlaka ya Spika.

Na Kwa kuwa, Siku ya tarehe 27 Januari, 2016 baadhi ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni walifanyavurugu na   kudharau mamlaka ya Spika.

 Na Kwa kuwa,Mheshimiwa Spika alipeleka suala la baadhi ya wabunge hao kufanya vurugu na kudharau mamlaka ya Spika kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kuwataja majina Wabunge wafuatao:-


i)                   Mhe. Godbless J. Lema, (Mb)
ii)                 Mhe. Pauline Gekul, (Mb)
iii)               Mhe. Ester A. Bulaya(Mb);na
iv)             Mhe.Tundu Antiphas Mughwai Lissu,(Mb)

Na kwa kuwa pia,Spika aliwasilisha majina mengine matatu siku ya tarehe 10 Machi, 2016 ili Kamati iweze kufanya uchunguzi kuhusu ushiriki wao katika vurugu  zilizotokea siku tajwa hapo juu. Majina ya Wabunge walioongezwa ni hawa wafuatao:-

(i)                           Mhe. Kabwe Zuberi. Ruyagwa Zitto, (Mb)
(ii)                         Mhe.John W. Heche (Mb), na
(iii)                       Mhe. Halima James Mdee, (Mb)

Na Kwa Kuwa, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilikaa kati ya  tarehe 07Machi, 2016 hadi tarehe 12 Machi, 2016 Jijini Dar es salaam kabla ya kuahirishwa kwa muda kutokana na wajumbe wa Kamati hii kuwa wajumbe wa Kamati za kisekta ambazo Wajumbe walitakiwa  kuhudhuria vikao vya Kamati.  Kamati ilirejea tena tarehe 16 Mei, 2016 hadi tarehe 29 Mei, 2016 na kufanya uchunguzi wa shauri hili. Kamati iliweza  kubaini kuwa, Wabunge wafuatao wamevunja masharti ya Kifungu cha 24(c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya  72 (1) 68 (10),60(2)&(12) na 74 (1)(a) na (b) kwa kusimama na  kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.

(i)                           Mhe. Tundu Lissu, (Mb)
(ii)                         Mhe. Halima Mdee, (Mb)
(iii)                       Mhe. Pauline Gekul, (Mb) na
(iv)                      Mhe. Ester Bulaya,(Mb)

Na kwa kuwa,Mhe. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto(Mb), alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2)na (12), 74(1) (a) na (b) na kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika
Na kwa KuwaMhe. Godbless Lema(Mb) alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296pamoja na Kanuni ya 74(1)(a) na (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kudharau Mamlaka ya Spika.
Na kwa kuwa,Mhe. John Heche(Mb) alivunja Kanuni ya 72(1) na 68(10) ya Kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo lilikwishatolewa Mwongozo.
Na Kwa Kuwa, vitendo hivyo visivyo na tija, vilivuruga shughuli za Bunge zilizokuwa zikiendelea na kuathiri heshima ya Bunge Mbele ya Umma wa Watanzania jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.



Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:
(a)           Wabunge wafuatao:

(i)  Mhe. Ester A. Bulaya, (Mb) na
(ii) Mhe. Tundu A. Mughwai Lissu(Mb)

wasihudhurie vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki  kuanzia tarehe 30 Mei, 2016pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika na pia walihusika kwa kiasi kikubwa kuchochea vurugu zilizotokea siku ya tarehe 27 Januari, 2016.
Aidha, Bunge linaazimia kuwa:

(b)           Wabunge wafuatao:

i)             Mhe. Pauline Gekul (Mb)
ii)           Mhe. Godbless Lema(Mb)
iii)         Mhe. Kabwe Zuberi  Ruyagwa  Zitto(Mb) na
iv)       Mhe. Halima James Mdee(Mb)

Wasihudhurie vikao vyote vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyosalia kuanzia tarehe 30 Mei, 2016 kwa kuwa walifanya vitendo ambavyo ni vya utovu wa nidhamu na dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika. Vitendo hivyo vya vurugu walivyovifanyavilisababisha kuvurugika kwa Shughuli za Bunge.
Vilevile Bunge linaazimia kuwa:

(c)           Mhe. John W. Heche (Mb)

Asihudhurie  vikao Kumi  mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja kuanzia tarehe 30 Mei, 2016.Adhabu hiyo kwa Mhe. John Heche (Mb) imezingatia kwamba alipatikana na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa Kamati kwa kutii wito wa Kamati wa Kufika na analiju  maswali yote kama yalivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya Kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.

KWA HIYO BASI, kwa mujibu wa Kifungu cha 30A (1) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 74 (4) na (6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  linalokutana katika Mkutano wa Tatu, linapokea na kukubali adhabu inayopendekezwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa Wabunge waliofanya vurugu siku ya tarehe 27 Januari, 2016  na linaazimia kupitisha mapendekezo ya adhabu kwa Wabunge husika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na kutoa hoja.

Kapt.(Mst). George H. Mkuchika, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE
30 Mei, 2016

      

No comments:

Post a Comment