Bunge limepitisha Miswada ya Sheria
ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Rasilimali na Maliasili ya
mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika
Mikataba inayohousu Rasilimali na Maliasili za Nchi ya mwaka 2017.
Miswada hiyo iliyoletwa Bungeni kwa
Hati ya Dharura iliwasilishwa Bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa
Paramagamba Kabudi na kujadiliwa kwa siku moja.
Kabla ya kuwasilishwa Bungeni
Miswada ya Sheria hizo ilijadiliwa na Kamati ya Bunge ya Pamoja huku wadau
mbalimbali wakipata fursa ya kutoa maoni yao.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa
kwa Sheria hizo, Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai alisema Bunge
limeshafanya kazi yake kwa miswada hiyo kwa hatua zake zote na kwamba
kilichobaki ni kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais ili iweze iliweze kusainiwa kwa
mujibu wa Ibara ya 97 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
“Niwapongeze sana Wabunge mliofanya
kazi bila kuchoka,pongezi kwa Kamati ya Pamoja ya Bunge,Chini ya Mwenyekiti
Mheshimiwa Doto Biteko, Miswada ilipelekwa kwenye Kamati Nne, jambo ambalo
katika Bunge la 11 ni mara ya kwanza, zaidi ya Wabunge 100 waliipitia kifungu
kwa kifungu na hatua kwa hatua,” alisema.
Mheshimiwa Spika pia aliwapongeza
wadau wote waliofika Bungeni Dodoma kwa ajili kutoa maoni yao yaliyosaidia
kuboresha muswada hiyo.
“Naipongeza pia Serikali na kipekee
Mheshimiwa Kabudi kwa ushiriki wake mkubwa katika jambo hili, jinsi ambavyo
yeye na timu yake wamefanya kazi usiku na mchana,” alisema
“Kuna maeneo ambayo Serikali ilileta
Jedwali la Marekebisho maana yake ni kwamba imeyakubali maoni yaliyotolewa na
imeboresha hii ni ‘spirit’ nzuri kwa Serikali, tunaipongeza kwa kukubali
kuwasikiliza Wabunge na Wadau,” aliongeza Spika
Aidha, alisema Miswada hiyo miwili
imeliingiza Bunge la 11 katika hisrtoria ya kipekee na kwamba kama spika wa
Bunge anajisikia faraja kwa kuingia katika historia hiyo mpya ya kuangalia
maliasili ya nchi kwa kuweka sheria ya Watanzania kuimiliki na kuweka taratibu
za mikataba zilizopigiwa kelele kwa muda mrefu.
“Hatua hii ni kubwa tunaipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano, kama tukiona kuna matatizo, Serikali ipo na sisi
Wabunge tupo,tutakaa na kuona jinsi ya kuweka vizuri zaidi,” alisema.
No comments:
Post a Comment