Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Zubeir Ali
Maulid amewataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa waliyoipata
ya kuwa wenyeji wa Mkutano wa 50 wa
Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), Kanda ya Afrika kujitangaza kibiashara na
kitalii.
Mheshimiwa Maulid ametoa rai hiyo leo Kisiwani Zanzibar
wakati akikagua maandalizi ya Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe
30 Agosti hadi septemba 5 mwaka huu katika Hoteli ya Madinat Al Bahr Business
& Spa.
Alisema mkutano huo kufanyika Zanzibar utafungua fursa katika
sekta za biashara ikiwemo utalii na kuwataka Watanzania kuonyesha ukarimu kwa
wageni hao.
“Tuonyeshe ukarimu wakati kupokea wageni hawa, tuitendee haki
nchi yetu, tukikaa nao vizuri wageni wetu itatosha kwa sisi kujitangaza,
tutumie fursa hii kwa kadri tutakavyoona inaweza kuisaidia nchi” alisema.
Alisema mkutano huo ni wa kihistoria kwa kuwa unaweza kuvunja
rekodi ya mahudhurio ya wajumbe zaidi ya 400 kutoka nchi 18 wanachama ambao unajumuisha
maspika, manaibu spika na wabunge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CPA, Tawi la Zanzibar, Mheshimiwa
Simai Mohammed Said alisema mkutano huo mbali na kutoa fursa za kiuchumi lakini
pia utawezesha wajumbe kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao
ikiwemo kuisimamia Serikali katika mambo yanayogusa wananchi.
Awali akizungumzia maandalizi ya awali, Katibu Msaidizi wa
CPA, Kanda ya Afrika, Said Yakubu alisema Nchi zote 18 wanachama zimethibitisha
ushiriki na kwamba maspika 23 kutoka mabunge makubwa na madogo watahudhuria.
Alisema nchi wanachama wa CPA, Kanda ya Afrika ni Botswana,
Cameroon, Eswatini, Ghana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji,
Namibia, Nigeria, Rwanda, Seychelles, Siera – Leone, Afrika ya Kusini,
Tanzania, Uganda na Zambia.
No comments:
Post a Comment