WELCOME TO TANZANIA NATIONAL ASSEMBLY OFFICIAL BLOG: CONTACT US: P.O.BOX 941 DODOMA, TANZANIA, WEBSITE: parliament.go.tz , FIND US ON FACEBOOK >>> www.facebook.com/bungetz1, FOLLOW US ON TWITTER >>> @bunge_tz.>>>KARIBUNI

Thursday, August 29, 2019

SPIKA WA BUNGE MHESHIMIWA JOB NDUGAI AKARIBISHA USHIRIKIANO NA NCHI YA IRELAND

Spika wa Bunge Mheshimiwa, Job Ndugai ameishukuru Serikali ya Ireland kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ya sheria na haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika ametoa shukrani hizo leo ofisini kwake Bungeni JIjini Dodoma wakati alipokutana na Ujumbe wa Wanasheria wa haki za binadamu kutoka Ubalozi wa Ireland wakiongozwa na Naibu Balozi wa Ireland hapa nchini Mheshimiwa Bronagh Carr.
Alisema Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano huo na Serikali ya Ireland katika masuala hayo ya sheria pamoja na kudumisha haki za binadamu.
Aidha, alisema upo umuhimu ujumbe huo, ukakutana na Umoja wa Wabunge Wanawake nchini (TWPG) ili kujadili changamoto za kijinsia zilizopo katika maeneo yao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuwa Ireland imepiga hatua kubwa kwenye masuala ya usawa wa kijinsia.
aliwataka pia wakutane na  Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambapo miswada yote inayoathiri huduma za jamii ikiwemo masuala ya elimu na jinsia hujadiliwa kwenye kamati hiyo kabla ya kuingia Bungeni.
“Katika suala la usawa kwa jinsia Bunge letu limepiga hatua kubwa ambapo Wabunge wa Viti Maalum Wanawake ni asilimia 30 ya Wabunge wote 393 pia wapo Wabunge wa majimbo ambao ni Wanawake hivyo kuongeza nafasi ya uwakilishi wa jinsi hiyo Bungeni” alisema Mheshimwa Spika.
kwa upande wake Kaimu Balozi wa Ireland, Mheshimiwa Bronagh Carr alimshukuru Mheshimiwa Spika kwa kukubali kukutana nae pamoja na Kamati za Bunge.
Alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland umekuwepo kwa kipindi cha miaka 40 na unazidi kuimarika siku hadi siku.
Ujumbe huo umelenga kukutana na wadau mbalimbali wa masuala ya kisheria  ikiwemo Wabunge, Mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali pamoja na Jeshi la polisi nchini ili kuimarisha ushirikiano katika masuala ya sheria na jinsia.
Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai akisalimiana na Naibu Balozi wa Ireland hapa nchini walipokutana na kufanya mazungumzo Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma hii leo. 
Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai akifafanua jambo alipokutana na Ujumbe wa Wanasheria kutoka ubalozi wa Ireland nchini Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma hii leo.
Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Wanasheria kutoka ubalozi wa Ireland nchini waliomtembelea Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma hii leo.


No comments:

Post a Comment