Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai
amewataka watumishi wa Bunge kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa bidii.
Mhe. Spika alitoa rai hiyo kupitia
hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Spika, Mhe. Dkt. Tulia Ackson alipokuwa
anazindua Baraza la Wafanyazi la Ofisi ya Bunge lililofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge Tunguu Zanzibar.
Alisema kunahitajika mabadiliko
katika utekelekezaji wa majukumu ya kila siku kwa watumishi katika kuchapa kazi
ili kuleta utendaji kazi wenye tija na ufanisi.
Aidha, aliwataka wajumbe kupitia
mada zitakazowasilishwa katika Mkutano huo wa Baraza kukumbuka wajibu wao
katika kutelekeza majukumu waliyopewa kulingana na taaluma husika na hatimaye
kufanikisha utekelezaji bora wa majukumu na madaraka ya Bunge Kikatiba.
Vilevile, alimpongeza Katibu wa
Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai kwa kufanikisha utatuzi wa changamoto ya muda
mrefu ya muundo wa Ofisi ya Bunge ambayo hatimaye ufumbuzi umewezesha kuundwa
kwa Baraza la Wafanyakazi.
“Naomba
nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wote mlioteuliwa na Tume ya Utumishi wa
Bunge kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi na ni matumini yangu kwamba
mtatumia uwezo na karama mlizojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kutekeleza
majukumu yenu kwa ufanisi hivyo kuliwezesha Bunge kufikia malengo yake,” alisema.
Aliwapongeza pia Wajumbe na Wawakilishi
wa Idara na Vitengo kwa kuchaguliwa kushika nafasi hizo na kuwataka kutumia
nafasi zao ili kuwa kiungo kati ya Wafanyakazi wa kada, ngazi zote, Menejimenti
na Tume ya Utumishi wa Bunge.
Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi
ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na
Afya, TUGHE Ndugu Hery Nkunda na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Ndugu John Mchenya
ambao walinasihi Baraza kudumisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika ujenzi
wa nchi.
Awali akizungumza katika mkutano
huo, Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai alisema Ofisi ya Bunge imeunda
Baraza la Wafanyakazi baada kutokuwepo ya Baraza hilo katika kipindi kirefu
kutokana na changamoto zilizokuwepo za kimuundo za Ofisi ya Bunge.
Alisema, lengo la Baraza lililopo
kisheria ni kuboresha utendaji kazi wa
taasisi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na bila ya ugomvi wala mifarakano.
Kabla ya uzinduzi wa Baraza la
Wafanyakazi, wajumbe walimchagua Ndugu Frank Mbilinyi kuwa katibu wa Baraza na
Ndugu Felister Njovu kuwa Katibu
Msaidizi.
No comments:
Post a Comment