Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufungamanisha sekta za kilimo na nishati kupitia mikakati mbalimbali ya kukuza uchumi inayotekelezwa kwenye nchi hizo.
Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa 51 wa Jukwaa la Mabunge
ya SADC, unaoendelea Jijini Lilongwe nchini Malawi, Dkt. Tulia amebainisha
umuhimu wa kufungamanisha sekta hizo ili ziwezeshe ukuaji wa uchumi katika
ukanda wa SADC.
“Endapo tunahitaji nchi zetu ziweze kujitegemea kwenye suala la
usalama wa chakula, tunapaswa kujifunza kupitia nchi zingine zilizofanikiwa
katika sekta hii kama zilivyoainishwa kwenye taarifa ya kamati ya Chakula.”
“Tunapaswa kuweka kipaumbele kwenye miundombinu wezeshi
itakayosaidia kukuza sekta ya kilimo, kama ni sekta ya nishati basi twende
pamoja kama Jumuiya kuhakikisha inakuza kilimo chetu,” amesema.
Akitolea mfano nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe.
Spika amesema “Nakubaliana na wenzetu wa Kongo kuwa mradi wa umeme wa maji wa
Inga unaweza kutoa umeme kwa nchi zote za SADCna hivyo kusaidia katika juhudi
za kukuza sekta ya kilimo.”
Dkt. Tulia amewaomba wajumbe wa Mkutano huo kuweka nguvu kwenye
maeneo mengine ya kiuchumi yatakayofungamanishwa ili kukuza sekta ya kilimo
kabla ya kufikiria kupata wawekezaji wakubwa watakaokuja kuwekeza katika sekta
hiyo.
Aidha, Dkt. Tulia ametoa wito kwa wajumbe hao kuzishauri nchi
zao kuondoa vikwazo katika biashara ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwa
wingi miongoni mwa nchi hizo kama sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya kilimo.
Kadhalika, Mhe.Spika ameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa
biashara baina ya nchi hizo ili kuhakikisha kunakuwapo na soko la uhakika kwa
mazao yanayozalishwa na wakulima.
“Iwapo nchi mojawapo katika ukanda huu inazalisha kwa wingi zao
fulani, kwanini nchi zingine wanachama zisiiunge mkono kwa kununua zao hilo
badala ya kwenda kununua katika nchi zilizo nje ya Jumuiya ya SADC,kwa kufanya
hivyo tutatengeneza soko la ndani la bidhaa za kilimo,”amesema
Awali, Mjumbe wa Jukwaa hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya SADC PF ya Chakula, Kilimo na Maliasili, Mhe.Ishmael Onani amewasilisha
Taarifa ya Kamati hiyo iliyobeba Kaulimbiu ya Ushiriki wa Mabunge katika ujenzi
wa mifumo imara ya kilimo kupitia usimamizi wa fedha za umma.
Amesema, pamoja na ukweli kwamba kilimo ni kati ya sekta muhimu za kukuza uchumi na kupunguza umaskini lakini kumekuwa na uwekezaji mdogo kwenye sekta hiyo jambo linalosababisha ukuaji hafifu wa uchumi kwa nchi za SADC.
No comments:
Post a Comment