RAIS WA IPU AWAOMBA WATANZANIA USHRIKIANO ILI KUONESHA UTOFAUTI
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)
Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ameomba ushirikiano kutoka kwa Watanzania wote ili
kuionyesha Dunia utofauti wa Tanzania kuishika nafasi hiyo.
Dkt. Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la
Tanzania ametoa kauli hiyo leo Bungeni Dodoma katika halfa ya kumpokea akitokea
Nchini Angola ambako alishinda nafasi ya Rais wa IPU katika uchaguzi uliofanyika
Oktoba 27, 2023.
Amesema Tanzania inayo nafasi ya kufanya vizuri
katika nafasi hiyo iwapo kutakuwepo ushirikiano kutoka kwa watu wote.
“Nafasi hii ni yetu wote, ukiwa na ushauri wa
namna ya kuupeleka umoja huu mbele tuletee ili tufanye vizuri, usisuburi
tushindwe.
“Ifike mahali tukitaka nafasi nyingine
kimataifa tupate kwa kuwa tulifanya vizuri kwenye hii, tutasikiliza ushauri
wenu, ninaamini tutafanya vizuri na Dunia itajua kwamba tulishawahi kushika hii
nafasi, viongozi wa dini muendelee kutuombea,” alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania kuondoa tofauti zao kwenye
masuala ya uwakilishi wa Tanzania Kimataifa kwa kuacha kuidharau nchi mbele ya
nchi nyingine.
“Nafasi kama hizi siyo za kuzipiga teke,
tujitahidi kujizuia hasa katika mambo ya kimataifa, tusifike mahali ya kuiuza
au kuidharau nchi yetu kwa wengine, usiungane na adui kwa ajili ya kulipiga Taifa
lako,” alisema.
Mheshimiwa Dkt. Tulia alitoa shukrani kwa
Mwenyezi Mungu kwa kumuwesha kupita katika mchakato wa uchaguzi uliodumu kwa
miezi mingi na kwamba isingiwezekana bila yeye kutoa kibali.
“Vilevile namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Hasan Suluhu kwa kuridhia nigombee nafasi hii, nafasi kama hii huwezi kugombea
bila nchi yako kuruhusu na anayeruhusu ni Mheshimiwa Rais.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais
kwa kuridhia Bunge la Tanzania kuchukua nafasi hii, pia niwashukuru wote
walioshiriki kwa nafasi yao, kwa maombi, maoni, kututia moyo na michango ya
kifedha pamoja na waliotukatisha tamaa kwa kuwa ilitufanya tupige hatua kwa
haraka zaidi” alisema.
Alisema Mheshimiwa Rais pamoja na kutoa usafiri
wa ndege kumrudisha Tanzania, lakini pia ametoa ushirikiano mkubwa ambao ndiyo
umemfikisha hapo toka mchakato wa uchaguzi ulipoanza.
“Hatukuwa peke yetu, wapo marafiki wengine
walikuja kutusaidia ili tushinde nafasi hii, tumeungwa mkono na mataifa mengi
kwa kuwa wanaamini sera za nchi yetu ambazo zinaendana na misingi ambayo IPU
inaisimamia,” alisema
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Tulia alieleza historia
yake kwa ufupi akitambua mchango wa Mheshimiwa Balozi Dkt. Asha Rose Migiro
katika mafanikio yake huku akiahidi kuandika kitabu.
Waziri
Mkuu
Awali Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim
Majaliwa akitoa salamu za Serikali
alisema Mheshimiwa Rais Samia Hasan Suluhu, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi na
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wanampongeza kwa ushindi mnono wa nafasi hiyo
nyeti.
“Sisi tumefarijika kama Serikali kwa sababu moja
kati ya majukumu yako utakuwa unashiriki vikao vyote vya Umoja wa Mataifa, tunayo
mikataba mingi katika nyanja za kimataifa, tutakutumia wewe kuingiza ajenda za
nchi.
“Tuna uhakika utatupigania, tulikuwa
tunakufuatilia katika mchakato wa kuomba kura, kazi kubwa mmeifanya leo
tunifurahia kazi hii.
“Mheshimiwa Rais amefurahishwa na akaamua
kukuletea ndege kubwa kwa ajili yako na kwa ajili ya ya heshima uliyoileta
nchini. Naahidi Serikali itashirikiana na wewe kila hatua, na maeneo ambayo
utahitaji Serikali ikupe taarifa kwa ajili ya kwenda kufanyia kazi huko katika
majukumu yako tutakupatia,” alisema.
Naibu Spika
Mheshimiwa Naibu Spika, Mussa Azan Zungu
alisema mambo matatu ndiyo yalimfanya Mheshimiwa Dkt. Tulia kushinda nafasi
hiyo ambayo ni kujiamini, heshima na ukweli huku akisema jambo kubwa zaidi ni
kumuamini Mwenyezi Mungu na msaada kutoka kwa Mheshimiwa Rais.
“Sisi tuliogopa uchaguzi lakini Mungu
alishasema tunashinda, you deserved it (ulistahili) na umefanya kazi
kubwa sana,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed aliungana
na wengine wote kumpongeza Dkt. Tulia kwa kuwa Rais IPU wa kwanza mwanamke kutoka
Afrika.
“CCM imefarijika sana
kupata kiongozi katika nafasi hiyo, nifahari kubwa kwa wanawake wote Barani Afrika
hususan wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, kuchaguliwa kwa Dkt. Tulia kunaiweka
Tanzania kileleni katika ramani ya Dunia kwenye masuala ya demokrasia na usawa wa
binadamu kwa kuwa mwanamke kashika nafasi hiyo,” alisema.
Mheshimiwa Joseph Mhagama
Mheshimiwa Joseph Mhagama ambaye alikuwa mwenyekiti wa Timu ya Kampeni
aliwashukuru watu wote walioshiriki kampeni za kumnadi Mheshimwa Dkt. Tulia wakiwemo
wabunge sita wawakilishi wa IPU, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya kikanda na
kimataifa, mabalozi watatu na sekrearieti ya Bunge.
“Tunakuopongeza kwa kuleta heshima kwa Taifa, ushindi huu umechangiwa na
neema na baraka za mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais kwa kutoa baraka na
kuwezesha kwa hali na mali na ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki.
“Ubora wa mgombea wetu, sifa zake lukuki, weledi, maarifa na utaalamu wa
hali ya juu, haya yote yamewashinda wapinzani wake wote, sera ya mambo ya nje
na mahusiano ya diplomasia ambayo ni bora sana chini ya usimamizi wa Mheshimiwa
Rais imefanya kazi hii iwe nyepesi na umahili wa timu yetu ya kampeni.
Mheshimiwa Shally Raymond
Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Mheshimiwa
Shally Raymond alimpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia kwa niaba ya wabunge wote
wanawake .
“Shukrani kwa wazazi wako, Mungu alisema ukijitahidi utakuwa kichwa
huwezi kuwa mkia, nawasihi wazazi wengine wawalee Watoto wao vizuri ili tupate
kina Tulia wengi. Asante Mheshimiwa Rais kwa kukubariki hili, nakupongeza kwa
niaba ya wanawake wote, umeliheshimisha Bunge la Tanzania, Tanzania, Afrika na
Dunia kwa ujumla,” alisema.
Mheshimiwa Oran Njeza
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wate alisema wabunge wote walipokea
taarifa za ushindi wa Dkt. Tulia kwa furaja na vifijo.
“Shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kuitangaza Tanzania kidiplomasia, nina
imani hata IPU utaipaisha na utaonyesha utofauti.Umetupa matumaini makubwa na
sisi wana Mbeya tunajivunia,” alisema.
Katibu wa Bunge
Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi akizungumza katika hafla hiyo alisema
kwa ushindi alioupata Dkt. Tuliaunamuwezesha kuwa mkuu wa kisiasa wa chombo
hicho ambacho atakuwa akiongoza vikao vya maamuzi.
“Kwa nafasi hii aliyoipata Mheshimiwa Dkt. Tulia atakuwa akiiwakilisha
IPU katika mikutano na makongamano mbalimbali ya kimataifa. IPU inafanya kazi
kwa ukaribu na Umoja wa Mataifa (UN) hivyo Mheshimiwa Rais wa IPU atakuwa
anashiriki vikao vya UN.
“Tunaimani kwa uwezo na uzoefu wako utayatekeza majukumu yote uliyoanayo
kwa ufanisi na viwango, mimi na watumishi wenzangu tutafanya kila liwezekalao
kukuwezesha kutekekeza majukumu yako,” alisema.
------------------------------------
No comments:
Post a Comment