Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, Mhe. George Lubeleje
akiwahutubia Wauguzi wa Hospitali Teule ya Mvumi, Wilayani Chamwino Mkoani
Dodoma 14 Mei, 2016 wakati wa wakiadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani.
|
Na Benedict Liwenga, Dodoma.
Wauguzi Wilayani Chamwino pamoja na wengineo nchini wamepewa
pongezi kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa wa kutoa huduma ya afya kwa jamii ikiwemo
kuendeleza huduma hiyo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, Mhe.
George Lubeleje katika Hospitali Teule ya Mvumi
iliyopo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakati alipomwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa
Tanzania, Mhe. Job Ndugai ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku
ya Wauguzi Duniani.
Mhe. Lubeleje amesema kuwa bila kuwepo kwa wauguzi huduma ya
afya ingeyumba kutokana na ukweli kwamba Wauguzi hao ni zaidi ya asilimia 60 ya
Watumishi wote wa sekta ya afya ambapo wanatekeleza asilimia 80 ya shughuli
zote za afya.
Amefafanua kuwa, Wauguzi ndiyo wenye kuandaa mazingira mazuri
kwa daktari kutekeleza majukumu yake kwani baada ya daktari kumaliza kumuona
mgonjwa na kutoa maelekezo yake, muuguzi husimamia utekelezaji wa maelekezo
hayo pamoja na tiba na huduma kwa mgonjwa husika.
Ameongeza kuwa, mara nyingi muuguzi ndiye anayefanya kazi ya
kuuguza mgonjwa kwani wagonjwa wengi hutumia muda mwingi wakiwa mikononi mwa
wauguzi kuliko wanaoutumia mikononi mwa wahudumua wengine wa sekta ya afya.
Aidha, Mhe. Lubeleji amewapongeza wauguzi hao kutokana na
kaulimbiu yao katika Maadhimisho ya Wauguzi Duniani isemayo “Wauguzi;
Nguvu ya Mabadiliko: Uboreshaji wa uthabiti wa mifiumo ya afya” ambapo
amesema kwamba ni kaulimbiu katika wakati muafaka kwakuwa wauguzi wana nafasi
maalum katika maendeleo ya huduma ya afya na sekta yenyewe kwa ujumla.
“Ni chachu muhimu ya mabadiliko katika sekta ya afya, na
ndiyo rasilimali ya kuwawezesha uboreshaji wa uthabiti wa mifumo ya afya”,
alisema Mhe. Lubeleje.
Akifafanua baadhi ya changamoto zinazoikabili Hospitali Teule
ya Mvumi wilayani hapo, alisema kuwa Serikali inaelewa kuhusu mchango wa
wauguzi na inauthamini kwa kiasi kikubwa, vile vile amewahakikishia wauguzi hao
kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma wakiwemo
wa afya, hususani katika masuala ya mishahara na posho mbalimbali.
“Maombi yenu nimeyapokea na ninaahidi nitayawasilisha kwenye
Mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji, yale yanayotuhusu, kama Bunge
tutayachukua pia na kuisimamia Serikali ili iyatekeleze na hatimaye tuimarishe
huduma za uuguzi na afya kwa ujumla”, alisema Mhe. Lubeleje.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Farida Mgomi
amewasisitiza Wauguzi wilayani hapo kujituma kwa bidii katika kutekeleza
majukumu yao ya kutoa huduma ya afya kwa jamii kwani Serikali ya Awamu ya Tano
inahitaji mabadiliko yanayoendana na kasi ya “Hapa Kazi tu” kwa kuwahudumia
wananchi nchini.
Aidha, amewapongeza kwa juhudi zao na maarifa katika kazi yao
na kuwahakikishia kuwa Serikali itazidi kushirikiana nao katika kuleta
maendeleo katika sekta hiyo na kusimamia vema katika masuala yao mbalimbali.
Sikua ya Wauguzi Duniani huadhimishwa tarehe 12 Mei kila
mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mwanzilishi wa Uuguzi Bi. Florence
Nightngale aliyezaliwa tarehe 12 Mei, 1820 na kufariki mwaka 1910.
No comments:
Post a Comment