Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika akaunti zilizofunguliwa
kwenye benki mbalimbali za muda maalum (fixed) za Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA), zenye thamani ya Sh bilioni 440 zilizofunguliwa na riba
ndogo.
Agizo hilo
lilitolea mjini Dodoma na Kamati hiyo, wakati ilipomaliza kupitia na kujadili
hesabu za mamlaka hiyo za mwaka wa fedha 2014/15.
Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka, (Mb) amesema katika ukaguzi wa
mwaka ujao, CAG anatakiwa ashirikiane na Benki Kuu ya Tanzana (BoT) na Kitengo
cha Uchunguzi wa Fedha na kubainisha kiasi cha riba kilichokubaliwa na faida
iliyopatikana.
Mheshimiwa
Kaboyoka alizitaja benki zilizofunguliwa akaunti hizo na TPA kuwa ni NMB, CRDB,
Standard Charter na NBC.
Agizo hilo la
kamati limetokana na michango ya wajumbe wa kamati hiyo wakati wa kujadili
hesabu za TPA zilizokaguliwa na CAG na kubainika kuwepo kwa akaunti hizo lakini
zikiwa zimefunguliwa kwa riba ndogo tofauti na kiwango cha fedha hizo.
Mheshimiwa Kaboyoka,
alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kutokana na riba hiyo ndogo TPA
imepoteza mabilioni ya fedha, hivyo ni vyema ufanyike uchunguzi ili kubaini
kwanini benki hizo zimetoa riba hiyo ndogo kwa kiasi kikubwa cha fedha hizo.
Awali, wakati
akichangia katika mjadala wa kamati hiyo, Mbunge wa Msalala Mheshimiwa Ezekiel
Maige aliufafanisha ufisadi wa akaunti hizo kama ule wa Kishapu wa jumla ya Sh
bilioni tano ambao baada ya kusimamiwa ipasavyo fedha hizo zilipatikana.
“Kwa sasa wastani
wa chini viwango vya riba ni asilimia 7.5 na kiwango hicho huongezeka kutokana
na kiasi cha fedha ambacho mteja anaweka kwenye akaunti, Kimsingi TPA imepoteza
zaidi ya Sh bilioni 32, kwa makusudi kabisa na hii ni motive ya kifisadi,”alidai
Mheshimiwa Maige.
Kwa upande wa Mbunge
wa Magomeni Mheshimiwa Jamal Kassim Ally alishauri uchunguzi huo uihusishe na
BOT kwa kuwa ndio msimamizi wa taasisi za benki nchini na kuhakikisha hatua za
kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote walioshiriki kuiba fedha hizo.
Naye Mheshimiwa Aeshi
Hilal, alisisitiza kuwa pamoja na uchunguzi wa sakata hilo, lazima benki zote
zilizohusika na wizi huo wa fedha kupitia riba, nazo ziwajibishwe kwa
kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kilichopotea kinarejeshwa TPA.
Alisema katika
uchunguzi huo wa CAG pia ubainishe ilikuaje hadi benki hizo na TPA zikaingia
mkataba wa riba ndogo wa kiasi hicho kikubwa cha fedha tofauti na sheria za
fedha.
Pamoja na hoja
hiyo, wajumbe wa kamati hiyo pia walizungumzia tatizo la matumizi makubwa ya
mamlaka hiyo ya bandari wakati imekuwa ikichangia kiasi kidogo kwa upande wa
gawio la serikali.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa TPA Deusdedit Kakoko alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la
akaunti na kubainisha kuwa lilitokea katika utawala wa nyuma huku akisisitiza
kutekeleza maagizo ya serikali katika kutafutia ufumbuzi jambo hilo.
Kuhusu matumizi ya
mamlaka hiyo, alisema tayari TPA imeanza kudhibiti matumizi yake na kutolea
mfano kuwa inaweza kupunguza kutoka matumizi ya Sh bilioni 478 hadi kufikia Sh
bilioni 200.
Naye Msajili wa
Hazina, Lawrence Mafuru alisema tayari mamlaka hiyo imeanza kufanya vizuri
katika eneo la gawio kwa serikali kwani katika kipindi kifupi tangu bodi mpya
ianze utendaji, mamlaka hiyo imechangia serikalini kiasi cha Sh bilioni 150
kutoka Sh bilioni 12 za nyuma.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC)
wakipitia na kujadili Hesabu za mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) hiyo za mwaka
wa fedha 2014/15.
|
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari
nchini TPA, Deusdedit Kakoko akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali
zilizoibuliwa na wajumbe wa kamati ya PAC, katika kikao cha kamati hiyo mjini
Dodoma
|
No comments:
Post a Comment