Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Job Yustino Ndugai amesema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa (2005-2010) na Mbunge
Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samuel John Sitta
kilichotokea leo tarehe 7 Novemba, 2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini
Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa na Mwenyekiti wa
Bunge Mhe Azzan Mussa Zungu kabla ya kuanza kwa kipindi cha Maswali na Majibu ,
Mhe Spika amesema Mhe Sitta aliondoka nchini tarehe 3 Novemba, 2016 na alikuwa
nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu zaidi ambayo Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilikuwa inayagharamia.
“Waheshimiwa
Wabunge, kwa niaba yenu natoa pole nyingi kwa Familia hususan kwa Mbunge
mwenzetu Mhe Margareth Simwanza Sitta (Mb) wa Jimbo la Urambo ambaye
ameondokewa na Mumewe,” alisema Mhe Spika kupitia taarifa yake.
Pia Mhe Spika kupitia taarifa yake hiyo amewaeleza
Waheshimiwa Wabunge kwamba Ofisi ya Bunge itaendelea kuwapa taarifa zaidi
kuhusu msiba huu kadri itakavyokuwa inaendelea kuzipokea.
Kufutia taarifa hiyo kwa Wabunge, Bunge limetoa
heshima zake kwa Spika Mstaafu Mhe Samuel Sitta kwa Wabunge wote kusimama kwa
dakika moja kuomboleza kifo chake.
Aidha mara baada ya
kipindi cha Maswali na Majibu, Kamati ya
Uongozi ilikutana kwa dharura ili kujadili kuhusu hoja ya kuahirisha Bunge kufuatia
msiba huo ambapo Kikao hicho kiliridhia Bunge liahirishwe ili Waheshimiwa Wabunge
wapate muda wa kuomboleza.
Marehemu Samuel John Sitta enzi za uhai wake
akiongoza kikao cha Bunge akiwa kama Spika wa Bunge la Tisa (2005-2010).
|
No comments:
Post a Comment