WELCOME TO TANZANIA NATIONAL ASSEMBLY OFFICIAL BLOG: CONTACT US: P.O.BOX 941 DODOMA, TANZANIA, WEBSITE: parliament.go.tz , FIND US ON FACEBOOK >>> www.facebook.com/bungetz1, FOLLOW US ON TWITTER >>> @bunge_tz.>>>KARIBUNI

Tuesday, November 10, 2020

MHE. NDUGAI ACHAGULIWA KUWA SPIKA WA BUNGE LA 12



Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Y. Ndugai akijinadi wakati akigombea kuwa Spika wa Bunge la 12.

Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Y. Ndugai akiapa mara baada ya kuchaguliwa  kuwa Spika wa Bunge la 12.
Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Y. Ndugai akipokea vitendea kazi kutoka kwa Katibu wa Bunge, Ndg. Stephen Kagaigai mara baada ya kuchaguliwa  kuwa Spika wa Bunge la 12.
Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Y. Ndugai akipongezwa na Waheshimiwa Wabunge mara baada ya kuchaguliwa  kuwa Spika wa Bunge la 12.

Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Y. Ndugai akizungumza mara baada ya kuchaguliwa  kuwa Spika wa Bunge la 12.

 

Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12, umeanza kwa kumchagua Mbunge wa Kongwa, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) kuwa Spika wa Bunge hilo kwa kura 344 kati ya kura 345 zilizopigwa ushindi ambao ni sawa na asilimia 99.7.


Matokeo hayo yametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai katika kikao cha uchaguzi huo ambacho kiliongozwa na mwenyekiti wa muda, Mheshimiwa William Lukuvi.


Akizungumza mara baada ya kiapo, Mheshimiwa Ndugai aliwashukuru wabunge kwa ushindi huo wa kishindo huku akiwataka Wabunge wote hususani wale wapya kusoma Kanuni za kudumu za Bunge pamoja na Sheria mbalimbali zinazohusiana na Bunge.


"Muwe tayari kuchapa kazi kama kuna tatizo lolote msisite kuja kuniona bila wasiwasi wowote mimi nipo kwa ajili yenu wote,” alisema.


Aidha, alisema uwepo wa wabunge wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) haina maana kwamba Bunge hilo litakuwa Bunge la ‘Ndiyo Mzee’ na kuwataka wabunge hao wasisikilize maneno ya watu badala yake wachape kazi.


"Mimi nakataa kwamba kuwepo Wabunge wengi wa CCM humu ndani haimaanishi ndiyo kila kitu watu wataitikia ndiyo au hapana hapana utekelezaji wa majukumu utafanyika Kama kawaida.” alisema Mheshimiwa Ndugai.


“Hata hivyo mkiamua kuwa mabubu ili muonekane mna nidhamu shauri zenu kwani mtatoa majibu kwa wananchi waliowachagua muwasemee mambo yao baada ya miaka mitano,” alisema.


Mheshimiwa Ndugai aliwaambia Wabunge wa upinzani kwamba licha ya uchache wao Bungeni lakini wana haki zote kama Wabunge wengine hivyo na wao lazima wasikike.


Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa kwanza wa Bunge la Kumi na Mbili kimeendelea pia na uapisho kwa wabunge wateule.


No comments:

Post a Comment