Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Dodoma kuhusu kuanza kwa Mkutano wa Tano wa Bunge.
MHE SPIKA AZUNGUMZIA KUANZA KWA MKUTANO WA TANO WA BUNGE
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametangaza kuanza kwa
vikao vya Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 Mjini Dodoma kesho huku akitaja baadhi
ya shughuli zitakazofanywa katika Mkutano huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mjini
Dodoma, Mheshimiwa Spika alisema shughuli ya kwanza itakuwa ni Bunge
kukaa kama Kamati ya Mipango kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Kudumu za
Bunge ili kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Taofa unaokusudiwa
kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/ 2018.
Alisema katika mjadala huo wabunge watatoa ushauri kwa
Serikali kuhusiana na vyanzo mbalimbali vya mapato na vipaumbele vya kuzingatia
wakati Serikali ikiandaa bajeti ijayo.
“Mbali na shughuli hiyo vipindi vya Maswali na Majibu
vitakuwepo kama kawaida ikiwemo kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu
kinachokuwepo siku ya Alhamisi,” alisema Mhe Spika.
Alisema pia Katika Mkutano huu, Bunge litapokea Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na majibu ya
Serikali kuhusiana na taarifa hiyo.
“Pia Bunge litajadili taarifa Taarifa ya Kamati za Kudumu za
Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu
Hesabu za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka wa Fedha
2014/15
“Vievile Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itawasilisha
taarifa yake bungeni kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo,” alisema
Aidha, Mheshimiwa Spika alisema jumla ya miswada miwili ya
sheria itajadiliwa na kupitishwa ambayo ni Muswada wa
Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016(The Media Services Bill, 2016), na Muswada wa Sheria ya Marekebisho
ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa mwaka 2016 (The written Miscellaneous Amendments)
(No. 3) Bill, 2016).
Alisema kutakuwepo na semina kwa wabunge wote kuhusu Mkataba
wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi katika Nchi za Afrika Mashariki na
Jumuiya ya Ulaya.
Mwisho.
|