Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 3 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma, Juni 30, 2021.
-----
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
ili kuhakikisha bajeti ya 2021/2022 inatoa matokeo yaliyokusudiwa, Serikali itaimarisha matumizi
ya mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji na hivyo
kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuepuka malipo hewa na manunuzi ya umma
ya bidhaa na huduma zisizokidhi viwango vya ubora.
Ameyasema hayo leo (Jumatano,
Juni 30, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 12, Bungeni
jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka huu.
Amesema Serikali itahakikisha
uwepo wa thamani halisi ya matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa
miradi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki tena kwa wakati pale
inapobaini ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za
umma.
“Utekelezaji wa Mpango na
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 unakwenda sambamba na Mikakati ya
Serikali katika kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, utendaji na
uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wote wa sekta ya umma. Hatua hizo,
zinalenga kuhakikisha bajeti hii inatoa matokeo yaliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwasisitiza watendaji wa Serikali hususan wa Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wajipange vema na wahakikishe suala la
posho za madaraka kwa watendaji wa kata na vijiji kupitia mpango wa halmashauri
linasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe
wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya vijana na wafanyabiashara wadogo sambamba
na kuwapatia elimu pamoja na kuwashirikisha katika kubaini maeneo yanayoendana
na biashara zao. Amewaagiza watendaji hao wasikilize na kushughulikia kero
za wananchi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kutenga siku maalum kwa ajili hiyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema utaratibu wa utoaji wa vibali vya
ukaazi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki umesaidia kupunguza hatua za
kuchakata maombi kutoka siku 33 za hadi saba.
Amesema
kuwa kwa sasa waombaji hawalazimiki kwenda katika Ofisi za Kazi kwa sababu
taarifa zote zinapatikana kwenye mfumo na watajaza fomu moja tu ambayo huwa na
taarifa zote za kazi na ukaazi tofauti na awali ambapo wawekezaji walilazimika
kujaza fomu mbili.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge
la 12, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka huu.
Amesema miongoni
mwa manufaa yaliyopatikana kupitia matumizi ya mfumo huo ni kupungua kwa siku
za kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku 14 hadi siku tatu. “Hali
hii, pamoja na mambo mengine, imesaidia kupunguza malalamiko ya kuchelewa kupata
majibu ya maombi ya vibali vya kazi.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa
watumiaji wa mfumo kwa ajili ya maboresho na tayari imeshakutana na kupokea
maoni ya wadau wa ndani na nje kikiwemo Chama cha Wafanyakazi, Chama cha
Waajiri (ATE), Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi na
kuyajumuisha maoni hayo kwenye maboresho.
Amesema
Serikali inakamilisha maboresho ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Sura
436) kwa kuainisha maeneo yaliyokuwa na changamoto za kiutendaji na kuathiri
jitihada za kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini. Mfumo huo unatarajiwa
kuzinduliwa rasmi Agosti mwaka huu.
“Sambamba
na marekebisho hayo ya sheria, tangu tarehe 23 Aprili, 2021 tumeanza kutumia
mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kwa raia wa
kigeni na katika hatua za majaribio tayari maombi zaidi ya 500 yameshughulikiwa
kupitia mfumo huo.”